Kenya inapoadhimisha miaka 48 ya uhuru iliyonyakua kutoka Uingereza Disemba 12 1963, Wakenya wanatafakari na kujadili namna ya kutekeleza katiba mpya inayoleta mabadiliko makubwa ya kisiasa, kijamii, na haki za kiraia.
Mojawapo ya mabadiliko makubwa ni kuwaruhusu Wakenya wanaoishi katika nchi za nje kuweza kupiga kura katika uchaguzi unaofanyika nchini humo. Na mtihani mkubwa ni uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2012.
Kutokana na hali hiyo, maafisa wa tume ya uchaguzi na mipaka IEBC wakiongozwa na mwenyekiti wa tume Ahmed Issack Hassan, unatembelea miji mikubwa ya Marekani na kusikiliza maoni ya wananchi wa nchi hiyo, ili kutafakari namna ya kupanga zowezi hilo nje ya nchi kwa mara ya kwanza.